
Takriban watoto wanane waliofariki siku ya Jumamosi wameuawa na ndege zisizo na rubani usiku wa kuamkia katika mtaa wa mabanda unaodhibitiwa na genge katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.
Wakizungumza na shirika la habari la Associated Press siku ya jana Jumatatu, Septemba 22, 2025 jamaa na wanaharakati wamesema wengine sita walijeruhiwa vibaya katika shambulio hilo ambalo wamewalaumu polisi. Milipuko hiyo ilitokea katika eneo la Cité Soleil, ambayo inadhibitiwa na Viv Ansanm, muungano wenye nguvu wa genge ambao Marekani imeutaja kuwa shirika la kigeni la kigaidi.
Inaaminika kuwa shambulizi hilo la ndege zisizo na rubani lilikuwa likimlenga mshukiwa ambaye ni kiongozi wa genge hilo, Albert Steevenson, anayejulikana kama Djouma, ambaye alikuwa akijiandaa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa. Mtandao wa Kitaifa wa Ulinzi wa Haki za Kibinadamu wa Haiti ulisema kwamba Steevenson alikuwa akisambaza zawadi kwa watoto wakati shambulio hilo lilipotokea.
Romain Le Cour, mkuu wa Kitengo cha Uangalizi cha Haiti katika Mpango wa Kimataifa wa Kupambana na Uhalifu wa Kimataifa uliopangwa, amesema shambulio hilo linazua maswali ya dharura ya uwajibikaji. Akiuliza ni nani atachukua jukumu la shambulio hilo, na kuongeza kwamba shambulio hilo litaimarisha tu muungano wa magenge dhidi ya serikali.
Mtandao wa Kitaifa wa Kutetea Haki za Kibinadamu umesema raia watatu na washukiwa wanne wa genge hilo pia waliuawa katika shambulio hilo, huku watu saba wenye silaha wakijeruhiwa. Kikosi kazi kipya kilichoundwa mapema mwaka huu kinafanya kazi nje ya uangalizi wa Polisi wa Kitaifa wa Haiti na kinatumia ndege zisizo na rubani.
Haiti iko katika hali mbaya ya ukosefu wa usalama huku magenge yenye silaha yakidhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu. Shambulio hilo limetokea wakati kampuni ya usalama, Vectus Global, inayomilikiwa na aliyekuwa Mwanajeshi wa Jeshi la Wanamaji wa Marekani Erik Prince, ikitarajiwa kupeleka karibu watu 200 nchini Haiti kama sehemu ya mkataba wa mwaka mmoja wa kukomesha ghasia za magenge.
Kampuni hiyo ya binafsi inatarajiwa kuimarisha idara ya polisi isiyofadhiliwa na yenye wafanyakazi duni inayofanya kazi na polisi wa Kenya wanaoongoza ujumbe unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa unaohangaika kupambana na magenge.