Jumanne , 11th Oct , 2016

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kalima Ramadhani amesema Tume ya Uchaguzi nchini itafanya zoezi la kufanya marekebisho ya daftari la wapigakura kwa awamu mbili kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Kalima Ramadhani

Kailima ameyasema hayo katika kipindi cha HOTMIX kinachorushwa na EATV wakati akizungumzia zoezi linaloendelea la kutoa elimu kwa mpiga kura nchini, na kusisitiza kuwa hatua hiyo ya maboresha itasaidia kuongeza idadi ya watanzania wenye sifa za kupiga kura, kushiriki katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020.

Amesema katika awamu ya kwanza daftari hilo litaboreshwa katika mwaka wa fedha 2017/18, na kwa mara ya pili zoezi hilo litafanyika katika mwaka wa fedha 2019/20.

Kailima amesema tume hiyo imejifunza mengi kutoka katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2015 ambapo asilimia 32 ya watanzania waliojiandikisha kupiga kura na kuwa na sifa ya kupiga kura hawakufanya hivyo.

“Asilimia 32 ya wananchi waliokuwa na sifa za kupiga kura hawakufanya hivyo, ndiyo maana Tume ya Uchaguzi imeamua kuanza zoezi la kuelimisha wananchi katika maeneo mabalimbali kuhusu umuhimu wa kushiriki zoezi hilo” Amesema Kailima.

Tume ya uchaguzi nchini inazunguka katika taasisi mbalimbali kwa sasa zikiwemo shule, kwenye taasisi za dini pamoja na kwenye shughuli zinazokutanisha watu wengi kama kwenye Mbio za Mwenge wa Uhuru na kwenye vyombo vya habari lengo likiwa ni kuhakikisha elimu kwa wananchi inakuwa kubwa kuhusiana na umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi, pamoja na kutambua majukumu ya tume hiyo..