
Mkuu wa uchaguzi nchini humo Mahmood Yakubu amesema kwamba uchaguzi huo upo pale pale. Hilo linakuja licha ya onyo wiki moja iliyopita kwamba kuongezeka kwa ukosefu wa usalama kunaweza kulazimisha uchaguzi kufutwa au kucheleweshwa.
Profesa Yakubu alikuwa akizungumza katika hafla iliyoandaliwa na kituo cha mawazo cha Chatham House jijini London.
Raia wa Nigeria wanatarajiwa kumchagua rais mpya mwishoni mwa mwezi Februari, kisha watachagua magavana na mabaraza ya mitaa wiki mbili baadaye.
Chaguzi hizi zinafanyika wakati nchi hiyo ikikumbwa na visa vingi vya utekaji nyara, ujambazi, mivutano ya kidini na kikabila pamoja na vurugu za kupigania uhuru katika maeneo kadhaa ya nchi.
Kulingana na Prof Yakubu watu milioni 93.4 wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo, huku zaidi ya milioni 74 wakiwa na umri wa kati ya miaka 18 na 49.