"Niliogopa kumuuliza Mwinyi eneo la kumzikia" -JPM

Jumatano , 29th Jul , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amesema kuwa Serikali ilikwishatenga eneo maalum la maziko kwa viongozi wakuu wa Kiserikali watakaofariki, ambapo watazikwa Dodoma, kwa kuwa ndiko yaliko Makao Makuu ya Nchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli, akiwa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Julai 29, 2020, wakati wa shughuli ya mwisho ya mazishi ya Rais Mstaafu Hayati Benjamin Mkapa, ambapo amesema kuwa miaka kadhaa iliyopita Rais Mkapa kabla ya kufariki, alimfuata na kumuomba endapo ataaga Dunia, basi ataomba azikwe kijijini kwao Lupaso, ambapo aliogopa kumuuliza Mzee Mwinyi eneo atakalozikiwa kwa kuwa umri wake ulikuwa ni mkubwa zaidi.

"Kuna wakati Serikali ilipanga mahali pa maziko kwa viongozi na tulipangiwa kuwa tunazikwa Dodoma, Mzee Mkapa akaniuliza mlipanga maziko yawe Dodoma, mimi msinizike Dodoma nikasema wewe unataka wakuzike wapi akasema Lupaso, Mzee Kikwete akasema Msoga, nikaogopa kumuuliza Mzee Mwinyi kwa sababu alikuwa na miaka zaidi ya 90 na mimi nilisema nitazikwa Chato" amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameongeza kuwa, "Mkapa alipenda kwao, kwenye hili Watanzania tujifunze, Mzee Mkapa angeweza kuzikwa Dar es Salaam au Lushoto, lakini ndani ya dhamira yake alitaka azikwe mahali alipozaliwa katika kijiji cha Lupaso, najua Maaskofu mnaniangalia sana kwa sababu ninyi huwa mnazikwa kwenye makanisa".