Jumatatu , 12th Oct , 2015

Waziri mkuu Mh. Mizengo Pinda amewataka wananchi wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura Oktoba 25, mwaka huu, na kwamba wasiwe na hofu yoyote kwa vile serikali imejipanga vyema katika suala zima la ulinzi, ili uchaguzi huo ufanyike kwa amani.

Waziri mkuu Mh. Mizengo Pinda

Mh. Pinda amesema hayo mjini Sumbawanga, wakati alipokuwa anaongea na wakazi wa mji huo, na kusema kuwa kuna maneno yanayotamkwa na wanasiasa katika kipindi hiki cha kampeni ambayo yanachangia kuwatia hofu wananchi hasa wanawake, wayapuuze kwa vile kutakuwa na ulinzi wa kutosha.

Kitu kilichokuwa ni kivutio kikubwa sana kwenye mkutano huo, ni pale mzee Crisant Mzindakaya alipotangaza rasmi kumsamehe aliyekuwa mbunge wa Sumbawanga mjini na ambaye anatetea nafasi yake Aeshi Hilal, kwa uadui uliodumu tangu 2010 na kumnadi kwa kumuombea kura.

Mapema katibu wa CCM, wa mkoa wa Rukwa Bi. Rachel Ndegeleke amewatahadharisha watu watakaofanya fujo kwenye mkutano huo kuwa watachukuliwa hatua kali, baada ya kuonekana dalili hizo za fujo kufuatia Chama cha Demokrasia na Maendeleo nacho kuwa na mkutano wa kampeni jirani na maeneo hayo.