Jumatatu , 12th Jan , 2015

Mamia  ya  wananchi  wa  kijiji  cha  Kisangura wamechukua  mwili  wa ndugu yao na kuupeleka kituo cha polisi kwa madai kuwa polisi hao walihusika katika mauaji ya ndugu yao kwa kipigo.

Mwili wa marehemu ukiingizwa katika Kituo cha Polisi

Katika  tukio  lisilo  la  kawaida  mamia  ya  wananchi  wa  kijiji  cha  Kisangura wamechukua  mwili  wa marehemu  Samson  Nyakiha na kuupeleka  katika  kituo  kikuu  cha  polisi   cha  wilaya   ya  Serengeti mkoani Mara  baada  kudai  kuwa  ndugu  yao alifariki  dunia  katika  hospitali  ya  rufaa  ya  Bugando  kutokana  na kipigo  alichokipata  kutoka  kwa  askari  polisi  wa  wilaya  hiyo  kwa   kushirikiana  na  askari  wa  hifadhi  ya taifa  ya  Serengeti.
 
Ndugu  hao  wa  marehemu baada  ya  kuchukua  mwili  huo  katika  hospitali   ya  rufaa  ya  Bugando  walikwenda  moja  kwa  moja  hadi  kituo  cha polisi  na  kuingiza jeneza lenye  mwili   wa marehemu huyo  ndani, kisha  kuutelekeza na  kukusanyika  nje  ya  kituo  hicho  wakati  wakingoja  hatua  ambazo  zinachukuliwa  na  jeshi hilo kuhusu  watuhumiwa hao  wa mauaji.
 
Wakizungumza kabla ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa mara RCO Rogathe Mlasani  kufika na kuzungumza na  wafiwa  hao, wamesikitishwa na  askari hao kupiga ndugu yao  na kusababisha kifo  lakini  wakati wote  serikali imeshindwa kuchukua hatua.
 
Naye mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa  mara  RCO Rogathe Mlasani, akizungumza na wafiwa hao, pamoja na kuwapa pole, amesema jeshi la polisi  chini  ya ofisi yake litachukua hatua  za  haraka  za kuchunguza tukio hilo na kwamba  wahusika  wote  watakaobainika  watachukuliwa  hatua  kwa  mujibu wa sheria.
  
Kwa upande  wake   wakili  wa  upande  wa   wafiwa  Stephen  Magoiga, amewaomba wafiwa hao   kuwa  watulivu  wakati  wakisubiri  taarifa rasmi  za  jeshi la polisi  kama ilivyoahidiwa na mkuu huyo  wa  upelelezi  wa  makosa  ya jinai  mkoa  wa  Mara  kuwa taarifa  rasmi za uchunguzi  wa tukio  hilo  zitatolewa ndani  ya siku Saba.

Baada  ya  makubaliano  hayo  ndugu  hao  waliuchukua  mwili  huo  wa marehemu  na kwenda katika kijiji hicho cha kisangura  kwa  ajili  ya  mazishi.