
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkuu wa Wilaya hii ya Meatu, Fauzia Hamidu Ngatumbura, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Joelson Mpina, wamesema vifo vya watu, uharibifu wa mazao na nyumba unaosababishwa na wanyama hao wa mwituni, lazima vihitimishwe ili kujenga ustawi na maendeleo ya jamii ya pembezoni yenye usalama wa chakula.
"Watoto wa miaka chini ya 18 (wazazi) tunawatuma kulinda mashamba, tunawatuma kufukuza Tembo kwenye mashamba. Na matokeo yake vifo vyote vilivyotokea hapa, vilivyosababishwa na Tembo ni vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 16. Kweli ni mtoto wa Taifa, ni mtoto wako ni mtoto wetu sisi sote, lakini kinachotokea hatari yoyote hawezi kujihami, kwa nini tuendelee kuwatumia?" amesema DC Fauzia.
"Tumechoka kuona wananchi wakiendelea kulalamikia tatizo hili la Tembo kila wakati. Wananchi nyumba zao zimevunjwa, wananchi wameuawa, wananchi wamepewa ukilema, wananchi chakula chao kimeliwa kikiwa shambani na kikiwa majumbani. Tumeanzisha kujenga vituo vitatu vya kupambana na Tembo, (Vijiji vya) Ng'hanga, Mawilo na Mwamashimba-Mbugayabanhya, kuweka vituo.
Na katika vituo hivyo tutaweka magari matatu, kila kituo kitakuwa na gari na maaskari (askari wa wanyamapori). Lakini pia vijiji vya pembezoni huku tutaweka vijana watatu watatu ambao nao watakuwa wamepewa mafunzo," amesema Mpina.
Amesema mbinu za kisayansi zinazotolewa na mamlaka husika kukabiliana na dhahama ya wanyama hao, ikiwamo milipuko ya pilipilii na mizinga ya nyuki, uimarishwaji wa miundombinu ya barabara maeneo ya pembezoni unaofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, huenda ukawa maarobaini mwa changamoto hiyo.
"Tembo wapo huku, na saa nyingine hata wale opareta wale hawawezi kufika na gari. Lakini kwa sasa hivi kwa hizi barabara hizi na bahati nzuri sasa zipo kote pembezoni tumechonga barabara. Na hii hata kuchonga barabara huku pembezoni kote ni kuhakikisha kwamba tatizo hili la Tembo hili tunapambana nalo kwa njia hiyo. Kwa sababu kuna gari la kufukuza Tembo halafu haliwezi kuingia kufukuza Tembo na ukanda huu wote (vijijini Kisesa) haukuwa na barabara. Tunataka baadaye sasa tuanze kuchonga kutoka kitongoji kwenda kitongoji. Na mimi nataka nioneshe mfano," amesema Luhaga Mpina.