Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema linafanya uchunguzi wa taarifa za kutoweka kwa Mtawa Silianus Balyalemwa Korongo (49) Mkazi wa Mtaa na Kata ya Tungi, Manispaa ya Morogoro, ambaye ametoweka katika nyumba ya malezi ya Watawa wa Shirika la Ndugu Wadogo wa Franciscan (ORDER OF FRIARS MINOR -OFM ) tangu Disemba 1, 2025.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, aliyoitoa jana Disemba 3, 2025 imeeleza kuwa Jeshi hilo lilipokea taarifa za kutoweka kwa Mtawa huyo, ikieleza kwamba mara ya mwisho alitoka kwa ajili ya kwenda kununua Vifaa vya Ujenzi na hakurejea.
“Taarifa ya kutoweka kwake imefikishwa katika kituo cha Polisi Disemba 3, 2025 mchana ikieleza kwamba Mtawa aitwaye Silianus Balyalemwa Korongo (49) Mkazi wa Mtaa na Kata ya Tungi, Manispaa ya Morogoro ametoweka kutoka kwenye nyumba ya malezi ya Watawa wa shirika ndugu wadogo wa Watawa wa Shirika la Ndugu Wadogo wa Franciscan (ORDER OF FRIARS MINOR -OFM ) tangu Disemba 1, 2025,”taarifa hiyo imeeleza.
Kamanda Mkama amesema uchunguzi na ufuatiliaji unaendelea, huku Jeshi hilo likitoa wito kwa Mwananchi yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia kuhusu kutoweka kwa Mtawa huyo kuwasilisha taarifa hizo katika kituo chochote cha Polisi.

