Ijumaa , 12th Jul , 2019

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, limefanikiwa kuua majambazi wanne katika tukio la majibizano ya risasi, baina ya polisi na majambazi hayo huko eneo la Kwala, Wilaya ya Kipolisi Mlandizi.

Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa polisi mkoani humo, Wankyo Nyigesa, ambapo amesema, tukio hilo limetokea Julai 11,2019, majira ya saa 8 mchana baada ya kupata taarifa ya uwepo wa watu, waliopanga kwenda kuvamia na kupora fedha za malipo, kwa wafanyakazi wanaojenga Bandari Kavu ya Kwala.

"Jeshi la Polisi Mkoani hapa tuliweka mtego, na majambazi hao kujikuta wakinasa, na kuanzisha majibizano ya risasi na kupelekea majambazi wanne, kati ya sita wanaodhaniwa kuwepo kupoteza maisha" amesema RPC Wankyo.

Katika tukio hilo, majambazi hao wamekutwa wakiwa na bunduki mbili aina ya Pump action, Radio call moja, hirizi, dawa za kupulizia watu, kamba za kufungia watu na, Plasta za kuziba watu midomoni.

Vitu vingine ni pamoja na leseni za udereva, vitambulisho mbalimbali vya uraia, kadi ya bima ya afya, koti, kaniki, kanzu, suruali na kaptula .

Miili ya majambazi hao, imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa ya Tumbi.