Jumatano , 5th Oct , 2022

Wanafunzi kote Iran wameongeza maandamano kupinga vikosi vya usalama vinavyoripotiwa kuwapiga na kuwafunga macho waandamanaji katika chuo kikuu cha Iran.

Polisi na waandamanaji Iran

Polisi waliwakimbiza wanafunzi hao kwenye maegesho ya magari katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Sharif, kisha ikaripotiwa kuwapiga na kuwafumba macho. Video iliyothibitishwa na BBC inaonyesha vikosi vikiwangoja wanafunzi na kuwachukua kwa pikipiki.

Takriban watu 41 wamekufa tangu kuanza kwa maandamano hayo, wengi wao wakiwa waandamanaji lakini wakiwemo pia maafisa wa usalama wa Iran. Hii ni kwa mujibu wa idadi rasmi iliyotolewa, ingawa vyanzo vingine vinasema idadi halisi ni kubwa zaidi.

Shirika la kutetea Haki za Binadamu la Iran (IHR) lenye makao yake makuu mjini Oslo nchini Norway, limesema jana jioni kuwa idadi ya waliofariki ni angalau 57, lakini ikabaini kuwa kukatika kwa mtandao wa intaneti kunafanya iwe vigumu kuthibitisha vifo wakati maandamano hayo yanayoongozwa na wanawake yakiwa yameenea katika miji kadhaa.