Polisi waharibu mikakati ya CHADEMA

Friday , 29th Sep , 2017

Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoani Morogoro, Leonse Rwegasira amekiri kumkamata kisha kumuachilia Mbunge wa jimbo la Kilombero Peter Lijualikali wa Chadema pamoja na viongozi watatu wilayani Malinyi kwa tuhuma za kupanga kufanya kusanyiko

 lisilo halali.

Akizungumza na Mwandishi wa ukurasa huu, Kamanda Rwegasigira amesema kwamba wao kama jeshi la polisi kazi yao ni kushughulika na wahalifu au vitendo vya kihalifu hivyo kuwakamata viongozi hao wa Chadema ilikuwa ni kuzuia mipango ya kihalifu iliyokuwa ikipangwa.

"Sisi jeshi la polisi tunashughulika na wahalifu au wanaotekeleza matukio ya kihalifu. Ni kweli tuliwashikilia Lijualikali na wenzake watatu ambao walikuwa wakipanga kufanya kusanyiko lisilokuwa la halali jambo ambalo ni uvunjifu wa sheria. Tumewahoji na kuwaachia upelelezi bado unaendelea", amesema  Kamanda Rwegasigira

Ameongeza  "Sisi kama jeshi tunapokuwa kwenye oparesheni zetu huwa hatuangalii wadhifa ila tunashughulika na uhalifu, haijalishi wewe ni kiongozi wa dini au Mbunge, tunapokuwa tumepata taarifa za kihalifu kuhusu wewe tutakuchukua kwa ajili ya mahojiano. Hivyo kwa Lijualikali na wenzake tuliwakamata ili kuzuia hiyo mipango ya kutaka kufanya kusanyiko". 

Mbunge Peter Lijualikali

Hata hivyo Kamanda Rwegasigira amesema kwamba viongozi hao walipaswa kutoa taarifa polisi kuhusu mkutano waliokuwa wanatarajia kufanya na kuongeza kwamba na hata kama wangepatiwa kibali la kusanyiko na lengo la mkutano likawa kueneza hofu kwa watu basi kusanyiko lisingekuwa la halali

Hata hivyo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, amesema kuwa baada ya viongozi wake kukamatwa walipohoji waliambiwa kuwa viongozi hao walikamatwa kwa agizo la Mkuu wa Wilaya.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya Majura Kasika amesema ni kweli ameagiza polisi kumkamata mbunge huyo kwa kuwa anafanya siasa nje ya jimbo lake.

“Ndiyo, nimetoa maelekezo akamatwe maana hakuna mbunge anayeruhusiwa kufanya siasa nje ya jimbo lake” amesema Kasika.