
Polisi wa Indonesia wamerusha mabomu ya machozi kwa umati wa waandamanaji karibu na vyuo vikuu viwili katika mji mkuu wa eneo hilo, mashirika ya wanafunzi na viongozi yamesema leo Jumanne Septemba 2, na kuongeza mvutano mpya kwa maandamano mabaya ambayo yametikisa nchi tangu wiki iliyopita.
Baraza la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Bandung, kinachojulikana kama UNISBA, na Chuo Kikuu cha Pasundan kilicho karibu, zaidi ya kilomita 140 magharibi mwa Jakarta, ilisema kwenye Instagram kwamba mamlaka ilirusha vitoa machozi kwenye umati wa watu karibu na chuo hicho Jumatatu jioni.
Afisa wa polisi wa eneo hilo Hendra Rochmawan amesema mamlaka hazikuingia katika vyuo hivyo lakini ilijaribu kuwazuia waandamanaji wasio wanafunzi ambao walikuwa wakitafuta ulinzi ndani ya uwanja wa chuo kikuu, kwa sababu umati ulikuwa ukifunga barabara katika eneo hilo.
Wakati Mkuu wa UNISBA Harits Nu'man akiunga mkono taarifa ya polisi, na kuongeza kuwa chuo hicho kilikuwa kitovu cha matibabu kwa waandamanaji, Baraza la wanafunzi la UNISBA limesema kuwa vikosi vya usalama vilikishambulia kikatili chuo hicho, huku gesi ya kutoa machozi ikisababisha matatizo ya kupumua kwa baadhi ya wanafunzi na kuvituhumu vikosi vya usalama kwa kutaka kunyamazisha wapinzani.
Wanafunzi wa vyuo vikuu kwa muda mrefu wamechukuliwa kama vinara wa demokrasia ya Indonesia, ikiwa ni pamoja na kuchukua nafasi kubwa katika maandamano yaliyosaidia kumwangusha kiongozi wa kimabavu Rais Suharto mwaka 1998. Rais wa sasa, Prabowo Subianto, alikuwa kiongozi wa kijeshi chini ya Suharto.
Maandamano hayo yalianzia mjini Jakarta wiki moja iliyopita yakilenga matumizi ya serikali kama vile marupurupu yaliyoimarishwa kwa wabunge, na tangu wakati huo yameongezeka nchi nzima, huku kukiwa na ghasia na uporaji, baada ya gari la polisi kumgonga na kumuua dereva wa teksi ya pikipiki.
Takriban watu wanane wamefariki katika maandamano hayo, kutokana na taarifa ya Waziri Mkuu ya jana Jumatatu. Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yamekosoa mwitikio wa usalama kwa maandamano hayo.