Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamtafuta Helakumi Kacheri kwa tuhuma za mauaji ya mkewe yaliyotokea Januari 4, 2026 katika Kitongoji cha Tindegala, Kata ya Singisa, Wilaya ya Morogoro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama amesema katika taarifa kuwa tukio hilo lilitokea wakati marehemu akiwa shambani na mtuhumiwa.
Inadaiwa kuwa Helakumi alimshambulia marehemu kwa kutumia silaha kali sehemu mbalimbali za mwili, akimtuhumu kuendeleza mahusiano ya karibu na mzazi mwenza wake wa awali kabla ya mtuhumiwa kutoroka baada ya mauaji hayo.
Polisi wanachunguza matukio mawili ya vifo vilivyotokea katika Wilaya ya Kilombero na Wilaya ya Mvomero. Tukio la kwanza lilitokea katika Kitongoji cha Isago, Kata ya Mgeta, Wilaya ya Morogoro, ambapo mkulima Jesse Melumba (49) alifariki dunia akidhaniwa kuwa alikunywa sumu kwa bahati mbaya akiwa shambani. Uchunguzi wa awali umebaini uwepo wa mabaki ya dawa ya kilimo aina ya Banafos.
Tukio jingine liliripotiwa Januari 3, 2026 katika Kijiji cha Kata ya Doma, Wilaya ya Kilosa, ambapo mkazi Ally Charles Dagaza (38) alifariki dunia baada ya kukanyagwa na tembo wakati akilinda miche ya nyanya na zao la pilipili .
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limetoa wito kwa wananchi wote wenye taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa Helakumi Kacheri kujitokeza na kutoa ushirikiano kwa mamlaka ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mtuhumiwa.
