Muda mchache baada ya kuteuliwa kuwa Kaimu Rais wa Venezuela, Delcy Rodriguez aliyeidhinishwa na Mahakama ya Juu zaidi nchini humo kushika wadhifa huo ameishutumu operesheni ya Marekani iliyofanyika nchini humo na kutaka kuachiliwa kwa rais wa taifa hilo, Nicholas Maduro na mkewe.
Rodríguez aliteuliwa jana Jumamosi Januari 3 kama kiongozi wa muda wa Venezuela kwa mujibu wa Ibara ya 233 na 234ya Katiba ya nchi hiyo inayosema, kutokuwepo kwa rais ikiwa ni kwa muda au ni kwa kudumu, basi makamu wa rais ndiye anayechukua majukumu ya urais.
Rodríguez ambaye pia ni waziri wa fedha na wa mafuta, saa chache baada ya kukamatwa kwa Maduro na mke wake, Cilia Flores, aliongoza kikao cha Baraza la Kitaifa la Ulinzi, akiwa amezungukwa na mawaziri wengine na maafisa wakuu wa serikali, na kudai kuachiliwa kwa Maduro na mkewe mara moja, huku akilaani operesheni ya kijeshi ya Marekani.
Mbele ya bendera ya Venezuela, Rodríguez alisema operesheni hiyo ya alfajiri ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa na wa mamlaka ya Venezuela. Aliongeza kuwa hatua hiyo inapaswa kukataliwa na raia wa Venezuela na kulaaniwa na serikali kote Amerika ya Kusini.
Rodríguez amelielezea shambulio hilo kama uchokozi wa kijeshi usio na kifani wa Marekani, akisisitiza kwamba lilichochewa na nia ya kunyakua udhibiti wa hifadhi kubwa ya mafuta ya Venezuela akibainisha kwamba, serikali nyingi duniani kote zimeshangazwa na uvamizi huo wa Marekani dhidi ya taifa hilo.
Awali Rais Trump alihutubia waandishi wa habari kuhusu operesheni hiyo kutoka makazi yake ya Mar-a-Lago huko Florida akisema kwamba Marekani itaiongoza Venezuela hadi mpito salama wa kisiasa utakapofanyika.
Wakati huohuo, Shirika la ndege la Marekani limeruhusiwa tena kuruka juu ya anga ya Caribbean, baada ya kuzuiwa kufanya hivyo kutokana na uingiliaji kati wa kijeshi wa Marekani nchini Venezuela, hii ni kwa mujibu wa Waziri wa Uchukuzi wa Marekani Sean Duffy katika taarifa yake ya jana Jumamosi usiku.
Shirika la Usafiri wa Anga la Shirikisho la Marekani (FAA) lilikuwa limepiga marufuku mashirika ya ndege yaliyosajiliwa na Marekani kufanya kazi katika anga zote za Caribbean siku ya Jumamosi, kutokana na hatari za kiusalama ... zinazohusiana na shughuli za kijeshi zilizokuwa zinaendelea.

