Polisi washangazwa na kifo cha mtu Mwanza

Jumatatu , 13th Mei , 2019

Wakazi wa jiji la Mwanza wamekumbwa na sintofahamu baada ya kijana mmoja asiyefahamika kusadikiwa kujirusha kwenye jengo la ghorofa ya tatu katika  hoteli ya Gold Crest iliyopo jijini humo.

Kamanda Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro

Taarifa za awali za kifo cha kijana huyo zinaeleza kuwa baada ya kudondoka kutoka ghorofani, alipoteza maisha papo hapo.

Wakizungumza mapema asubuhi, wakazi wa mji huo wameonyesha kusikitishwa na kifo cha kijana huyo anayesadikiwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 30 ambae chanzo cha kifo chake hakijafahamika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amelizungumzia tukio la kifo cha kijana huyo akisema kuwa taarifa za awali walizozipata kuhusu tukio hilo hazikuwa za kweli kwa kuwa eneo ambalo inadhaniwa amejirusha na eneo ambalo umekutwa mwili wake ni tofauti.

"Haiingii akilini kuwa umbali ule ambao inadhaniwa mtu amejirusha na eneo la barabara ambalo amekutwa, haiwezekani pia mtu amejirusha akafika chini akawa mgongo wake mzima, kichwa kizima na hakuna hata tone la damu, kwahiyo kwa taarifa za awali, mimi nakanusha kuwa mtu huyu hajajirusha".

Tukio lingine kama hilo la mtu kujiua kwenye ghorofa katika jiji la Mwanza lilitokea December 21 mwaka jana ambapo mtu mwenye jinsia ya kiume alijirusha katika jengo la Rock City Mall.

Bonyeza hapa chini kutazama zaidi.