Hazard afanya maamuzi juu ya hatma yake Chelsea

Jumatatu , 13th Mei , 2019

Nyota wa klabu ya Chelsea, Eden Hazard, amezungumzia juu ya maamuzi yake ya mwisho juu ya kubakia ama kutobakia katika klabu hiyo msimu ujao.

Eden Hazard

Akiongea na mtandao wa Sun Sport, Hazard amesema, "nimeshafanya maamuzi yangu na nimeshawaambia viongozi wa klabu yangu wiki kadhaa zilizopita".

Tetesi zinaeleza kuwa Chelsea inahitaji pauni milioni 100 ili kumuachia mchezaji huyo, huku kocha wake, Maurizio Sarri akizungumzia undani wa taarifa hizo.

Baada ya kumalizika kwa mchezo wa mwisho wa ligi kati ya Leicester City na Chelsea, mchezo ambao uliisha kwa sare ya 0-0, Sarri alisema, "ninafahamu kuwa Eden Hazard alijitahidi kufanya kadri ya uwezo wake katika misimu 7 aliyodumu Chelsea. Amekuwa mmoja kati ya wachezaji wawili au watatu bora duniani".

"Lakini ninafikiri kwamba kwa sasa tunapaswa kumheshimu na kuheshimu maamuzi yake. Ni matumaini yangu na matumaini ya kila shabiki wa Chelsea kwamba atabakia na sisi, lakini kwa sasa sijui".

Inawezekana mchezo wa mwisho wa nyota huyo katika klabu ya Chelsea ukawa ni dhidi ya Arsenal katika fainali ya Europa League, Mei 29 mjini Baku, Azerbaijan.

Alipoulizwa kuhusu kutangaza maamuzi yake ya mwisho baada ya mchezo huo wa Europa League, Hazard alijibu, "ninafikiri hivyo, nimeshafanya maamuzi lakini sio ni kwa ajili yangu mwenyewe. Tuna fainali inafuata halafu tutaangalia".

Kwa muda mrefu hivi sasa, Hazard amekuwa akihusishwa kujiunga na miamba ya Hispania, Real Madrid, huku ikitajwa kuwa mchezaji huyo ni chaguo namba moja la kocha Zinedine Zidane. 

Eden Hazard ameshinda tuzo ya mpishi bora wa mabao katika EPL msimu uliomalizika, akiwa na jumla ya 'assist' 15, akifuatiwa na Ryan Fraser wa AFC Bournemouth mwenye 'assist' 14.