Ijumaa , 20th Sep , 2019

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Jumanne Murilo amezungumzia juu ya fujo zilizotokea leo katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza baina ya Kagera Sugar na mashabiki wa timu ya Alliance.

Kamanda Jumanne Murilo

Fujo hizo zilizuka baada ya Kagera Sugar kufanya mazoezi katika Uwanja wa Nyamagana ambao inadaiwa kuwa ulikuwa katika ratiba ya Alliance ambayo leo inatarajia kucheza na Biashara United.

Akizungumza na EATV & Radio Digital, Kamanda Murilo amesema, "leo ni siku ya mechi kati ya Alliance FC na Biashara United lakini nasikia kuna timu ya Kagera Sugar ipo hapa. Watu wanaofanya mazoezi ni hizi timu mbili zingine, wao Kagera wakaenda mahala hapo kwahiyo zikafanyika fujo kiasi".

"Nilichokifanya mimi nimeagiza OCD wa pale kufuatilia, hizo taarifa za kocha kuumizwa sijazifahamu. Sisi tunaanzia kuhoji kule kule na kuhusu hili tumeanzia kuhoji kulekule kujua nini shida", ameongeza.

Alliance FC inatarajia kucheza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara dhidi ya Biashara United katika Uwanja wa Nyamagana, kesho Kagera Sugar itacheza dhidi ya Mbao FC.