Jumapili , 12th Sep , 2021

Serikali imesema Vijana ni kundi tegemewa kwa Taifa kwani wanabeba dira ya Taifa kutokana na mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa hivyo wanapaswa kulindwa dhidi ya changamoto zinazowakabili zikiwemo UKIMWI na vitendo vya ukatili.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga

Hayo yalisemwa jana Jumamosi Septemba 11, 2021 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga wakati akizindua Programu ya ONGEA Kitaifa Jijini Dodoma yenye lengo kuwafikia Vijana nchi nzima kupata uelewa wa masuala ya Maambukizi virusi vya UKIMWI kupitia vyombo vya habari.

Katika uzinduzi wa programu hiyo TACAIDS inashirikiana na wadau wa maendeleo ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto (UNICEF) ambapo programu hiyo ni kampeni ambayo imetengenezewaa vipindi maalum vya redio ambavyo vina ujumbe unaowalenga vijana ili kuwezesha kundi hilo kutambua masuala VVU na Ukimwi vitakavyorushwakupitia East Africa Radio na Clouds Fm.

Naibu Waziri Ummy alieleza kuwa Uzinduzi wa programu ya kimataifa ya ONGEA ni fursa ya kuwafia vijana balehe nchini kupitia vyombo vya Habari ili kuwaongezea uelewa kuhusu matatizo na changamoto zinazowakabili katika Maisha yao ya kila siku ikiwemo maambukizi ya VVU ili wachukue hatua za kuandaa mikakati mbalimbali katika kukabiliana na changamoto hizo.

“Serikali kupitia uongozi wa Mheshimwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan tunaamini vijana ndio waliobeba taifa letu na ndiyo nguvukazi ya nchi kwa hiyo kwa pamoja lazima lazima tuhakikishe ushirikiano unakuwepo katika kulinda afya zao,” alisema Naibu Waziri Ummy.

Meneja wa Utangazaji wa East Africa Radio na TV, Lydia Igarabuza

Katika uzinduzi huo East Africa Radio iliwakilishwa na Meneja wa Utangazaji wa East Africa Radio na TV, Lydia Igarabuza, Afisa Mahusiano kwa Wateja wa East Africa TV na East Africa Radio, Nancy Mwanyika na Mtangazaji wa kipindi hicho kinachoruka kila Jumamosi, saa 6:00 Mchana ndani ya East Africa Radio Najma Paul.