Jumanne , 21st Feb , 2023

Rais wa Urusi Vladimir Putin amezungumza kwa kirefu kuhusu vita vya Urusi dhidi ya Ukraine katika hotuba ya hali ya taifa.

Katika hotuba hiyo amezilaumu nchi za Magharibi kwa kuchochea vita na kuvizidisha, akisema Marekani na washirika wake wanatafuta nguvu isiyo na mipaka.

Katika tangazo pekee kubwa, alisema anasitisha ushiriki wa Urusi katika makubaliano makubwa ya kudhibiti silaha na Marekani.  Hotuba hiyo imekuja kuelekea  maadhimisho ya kwanza ya uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine siku ya Ijumaa.

Wakati hayo yakijiri  Rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa kuweka wazi mtazamo wake kuhusu vita vya Ukraine kama vita vya demokrasia wakati wa hotuba yake baadaye Jumanne.

Atatoa hotuba yake katika mji mkuu wa Poland, Warsaw ikiwa ni siku moja baada ya ziara yake ya kushtukiza nchini Ukraine.