Pwani: Basi lapata ajali, abiria 18 wajeruhiwa

Jumatano , 12th Feb , 2020

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ACP Wankyo Nyigesa, amesema kuwa jumla ya watu 18 wamejeruhiwa katika ajali ya Basi la Saibaba lililogongana uso kwa uso na Lori asubuhi ya leo ya Februari 12, 2020.

Kamanda wa Polisi Pwani, ACP Wankyo Nyigesa

Kamanda Nyigesa amesema kuwa ajali hiyo imetokea katika eneo la kongowe na kusema kuwa majeruhi watano wamekimbizwa katika Hospitali ya Mloganzila kwa ajili ya matibabu na wengine wapo katika Hospitali ya Tumbi.

"Chanzo ni mwendokasi wa Lori uliopelekea kuligonga Basi la Abiria, Basi la Saibaba lilikuwa linatoka Sumbawanga kuelekea Dar es Salaam, hakuna vifo, majeruhi ni 18 na majina yao hayajafahamika kwasababu hawakuweza kuongea" amesema ACP Nyigesa.

Kwa mujibu wa Kamanda Nyigesa amesema kuwa Jeshi la Polisi, linajitahidi kufanya mawasiliano na kampuni ya mabasi hayo ili lilelete gari nyingine kwa ajili ya kuwachukua abiria walionusurika na kuwapeleka Dar es Salaam.