Raia kusindikizwa na Polisi Benki

Thursday , 14th Sep , 2017

Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni Murilo Jumanne Murilo amefunguka na kusema wananchi wanapaswa kulitumia jeshi la polisi wakati wa wakiwa wanakwenda kuchukua au kupeleka pesa zao benki ili kujihakikishia usalama wao pamoja na mali.

Kamanda Murilo Jumanne Murilo

Akizungumza leo asubuhi kwenye kipindi cha East Africa Breakfast, Kamanda Murilo amesema kuwa ni moja ya  jukumu la polisi kulinda mali za raia ndiyo maana kuna huduma inaitwa ' Money Escot'  hivyo wananchi wanapaswa kutambua wajibu wa kuchagua kuwa salama.

"Wezi siku zote wanatumia gharama kwa ajili ya kufanya uhalifu. Kama unajijua kesho nakwenda kuchukua kiasi kikubwa cha pesa au napeleka ni vyema ufikirie usalama wako. Fika kituo cha polisi kwa ajili ya kupatiwa huduma. Huduma hizi  sasa siyo kwamba tunahamasisha kila mtu mwenye fedha atake kusindikizwa, au kila mahali maana tunazingatia mazingira pamoja na kiasi unachokwenda kuchukua. Lakini niwasihi raia waweze kuzingatia sana usalama wao," Murilo

Pamoja na hayo Kamanda Murilo amewataka raia kutojisababishi uvamizi wenyewe kwa kuwatengenezea wahalifu fursa kama kujionyesha hadharani.

"Kuna mahali unaweza ukawa umekwenda lakini ukahitaji kutoa msaada na ni hadharani, Unaweza ukaomba pia huduma kwetu inaitwa 'Crowd Control' hivyo wananchi wanapaswa wao wenyewe kulitumia jeshi.  Lakini kuna wale wanaotaka kulipa bili ya elfu ishirini halafu anatoa milioni wezi hawatakuacha hata sisi hatuwezi kuja kukulinda na mitutu kwastaili kama hiyo. Heshimu usalama wako wenyewe," ameongeza