Jumapili , 26th Mei , 2019

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuwa atachukua walimu wa Tanzania kwa ajili ya kufundisha Kiswahili nchini kwake.

Rais Magufuli na Rais Ramaphosa

Rais Magufuli amehakikishiwa hilo leo, Mei 26, alipotembelea Ikulu Jijini Pretoria kufanya mazungumzo na Rais Ramaphosa, ikiwa ni siku moja baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi ya Afrika Kusini.

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli amempongeza Rais Ramaphosa kwa kuapishwa na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano wa kidugu na kihistoria na nchi hiyo, ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Nelson Mandela.

Katika salamu zake za kumshukuru Rais Magufuli kwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwake, Rais Ramaphosa amesema kufuatia uamuzi wa Afrika Kusini kuanza kufundisha Kiswahili, nchi yake itachukua walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania ili wafundishe somo hilo katika shule za msingi na sekondari nchini humo.