Alhamisi , 21st Mei , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ametangaza kuwa kuanzia Juni Mosi, 2020 vyuo pamoja na kidato cha sita vitafunguliwa kuendelea na masomo.

Rais Magufuli

Amesema hayo katika hotuba yake alipokuwa akiwaapisha Naibu Waziri wa Afya, mabalozi, Katibu Tawala na Mkurugenzi wa TAKUKURU leo Mei 21, Jijini Dodoma.

Amesema kuwa vyuo vyote viofunguliwe tarehe moja Juni na kuitaka Wizara ya Elimu na Wizara ya Fedha kuandaa utaratibu mzuri wa wanafunzi kupata mikopo watakapofika vyuoni na kuhusu wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari, utaratibu utatolewa hapo baadaye.

"Tumeamua sisi kama Serikali vyuo vyote vifunguliwa tarehe moja Juni, 2020. Niwaombe sana wizara zinahohusika hasa Wizara ya Elimu na Wizara ya Fedha ambayo inahusika katika kutoa mikopo, ina siku 9 zijiandae ili vyuo vitakapofunguliwa kusiwe na kero zingine", amesema.

"Ukianchana vyuo, vijana wa kidato cha sita walio katika mitihani yao nao warudi shuleni kuanzia Juni 1 na wizara ipange mpango mzuri ili wanafunzi wafanye mitihani yao bila kuathiri mpango wa kwenda Chuo Kikuu", ameongeza.

Aidha Rais Magufuli amesema kuwa kuanzia Juni Mosi shughuli za michezo, ikiwemo Ligi Kuu ya Soka, Ligi Daraja la Kwanza na Michezo ya Majeshi nazo zitarejea lakini kwa kuzingatia utaratibu hasa wa mashabiki kutazama, utakaotolewa na Wizara ya Afya.

Pamoja na hayo Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa COVID-19 kwani licha ya kupungua nchini, lakini bado upo hivyo tahadhari zinapaswa kuendelea.