Jumatano , 12th Dec , 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kwa niaba ya Serikali ameongoza zoezi la kusaini mkataba na kampuni ya Arab Contractors ya nchini Misri, ujenzi mradi wa kufua umeme wa maji wa Stieglers Gorge ambao unatarajiwa kuzalisha zaidi ya megawats za umeme 2100.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.

Makubaliano hayo yamefikiwa Ikulu Jijini Dar es salaam mbele ya viongozi mbalimbali wa kitaifa wakiwemo Spika wa Bunge, Jaji Mkuu wa Mahakama,  Mawaziri mbalimbali wa nchi pamoja na Waziri Mkuu wa Misri.

"Tumegundua kuwa mradi huu ndio inayoufaa nchi yetu kwa sasa kwasababu chanzo chake ni cha uhakika, kwa tathimini ya awali mradi utazalisha umeme kwa miaka 60 ijayo, na utagharimu trilioni 6.5".

"Mradi huu utaleta manufaa kwa nchi yetu faida nyingine ni kubwa sana, umeme wote tulionao kwa sasa utazidiwa na mradi wa rufiji, na tunategemea mradi huu utakapokamilika gharama ya umeme itapungua sana."

"Nafahamu kuwa wapo watu wanaodai kuwa mradi huu utaharibu mazingira, hiyo siyo kweli hata kidogo. Tunajua kuwa umeme wa maji unasaidia kutunza mazingira, lakini pia eneo litakalotumika ni dogo kulinganisha na ukubwa wa hifadhi," amesema Rais Magufuli.