Rais Magufuli awarudisha kazini mahabusu 8

Alhamisi , 18th Jul , 2019

Rais Magufuli amewarudisha kazini askari 8 wa kesi ya Madini ambao walikuwa mahabusu kabla ya jana kuachiwa huru na Mkurugenzi wa mashtaka nchini Biswalo Mganga.

Rais Magufuli

Akiongea leo Mkoani Dodoma katika Jimbo la Kongwa Rais Magufuli amesema amewaona askari wale sura zao zinajutia kosa walilofanya na kwakuwa DPP amewatoa yeye ameamua warudi kazini.

''Kwasababu walikuwa wameshafukuzwa kazini nimeamua warudishwe kazini, lakini iwe fundisho kwa askari wanaopenda kuomba rushwa wakiwa kwenye majukumu yao'', amesema Rais Magufuli.

Mkurugenzi wa mashtaka nchini Biswalo Mganga, alifuta kesi 75 zilizokuwa zinawakabili mahabusu na wafungwa mbalimbali katika gereza kuu la Butimba mkoani Mwanza.

Miongoni mwa kesi zilizofutwa na DPP jana Julai 17, 2019 ni kesi namba moja ya uhujumu uchumi ya mwaka 2019, iliyokuwa ikiwakabili askari polisi nane waliohusika na utoroshaji wa madini  kilo 319 yenye thamani ya shilingi bilioni 27, ambao ndio Rais Magufuli amewarudisha kazini baada ya kuwa wamefukuzwa.