Rais Magufuli azungumzia afya ya Mama yake

Jumamosi , 13th Apr , 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amesema licha ya Mama yake mzazi kwa sasa anaumwa lakini hana sababu ya yeye kuchelewa kuhamia Dodoma kutokana na ahadi ambayo aliitoa.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma wakati akizindua Mji wa Serikali ambapo amebainisha naada ya viongozi wakuu wa kitaifa kuhamia huko yeye yuko njiani kuhamia Dodoma.

Rais Magufuli amesema "nakuja Dodoma nilichelewa kidogo baada ya kuuguliwa na Mama yangu, ambaye mpaka sasa bado yupo hospitalini hawezi kuzungumza, hawezi kula lakini nawahakikishia nakuja Dodoma kwa sababu hakuna cha kunichelewesha kuja Dodoma."

Aidha Rais Magufuli ameongeza kuwa "wakati natoa ahadi wapo watu wachache ambao hawakuamini kama tutahamia Dodoma, na walikuwa na sababu ya kutoamini, kama tulishindwa kwa miaka 40, tungewezaje kwa miaka 3 lakini ahadi huwa ni deni."

Katika hatua nyingine Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali Mabeyo amesema kuwa "ndani ya nchi yetu kwa kushirikiana na vyombo vingine tutawalinda wananchi na mali zao, tutakabiliana na matishio ndani ya nchi yetu, na sasa hivi tunaendelea kufuatilia kauli tata zinazoashiria uchochezi na machafuko ndani ya nchi yetu"