Jumanne , 14th Oct , 2025

"Nililazimika kutafuta mahali salama pa kulinda maisha yangu," Rajoelina alisema katika hotuba yake ya usiku wa manane, ambayo ilichelewa kwa saa kadhaa baada ya wanajeshi kujaribu kudhibiti majengo ya shirika la utangazaji la serikali, ofisi ya rais ilisema.

Rais wa Madagascar Andry Rajoelina amesema aliikimbia nchi kwa kuhofia maisha yake kufuatia uasi wa kijeshi, lakini hakutangaza kujiuzulu katika hotuba iliyotangazwa na televisheni ya taifa jana Jumatatu kutoka eneo lisilojulikana.

Rajoelina amekabiliwa na wiki kadhaa za maandamano dhidi ya serikali yanayoongozwa na Jen Z, ambayo siku ya Jumamosi yalishuhudia kikosi cha wanajeshi wasomi kikijiunga na maandamano hayo na kuwataka rais na mawaziri wengine wa serikali kujiuzulu.

Hilo lilimfanya Rajoelina kusema kuwa jaribio haramu la kunyakua mamlaka lilikuwa likiendelea katika kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi na kuondoka nchini humo.

"Nililazimika kutafuta mahali salama pa kulinda maisha yangu," Rajoelina alisema katika hotuba yake ya usiku wa manane, ambayo ilichelewa kwa saa kadhaa baada ya wanajeshi kujaribu kudhibiti majengo ya shirika la utangazaji la serikali, ofisi ya rais ilisema.

Haya yalikuwa maoni ya kwanza kwa umma ya Rajoelina tangu kitengo cha kijeshi cha CAPSAT kugeuka dhidi ya serikali yake katika mapinduzi ya wazi na kuungana na maelfu ya waandamanaji waliokusanyika katika uwanja mkuu katika mji mkuu, Antananarivo, mwishoni mwa juma.

Rajoelina alitoa wito wa mazungumzo ili kutafuta njia ya kutoka katika hali hiyo na kusema katiba inapaswa kuheshimiwa. Hakusema aliondokaje Madagaska au alikokuwa, lakini ripoti ilidai kuwa alisafirishwa nje ya nchi kwa ndege ya kijeshi ya Ufaransa.

Maandamano ya kuipinga serikali, ambayo yalianza Septemba 25 kutokana na kukatika kwa maji na umeme kwa muda mrefu, yamesababisha hali ya umma kutoridhika dhidi ya Rajoelina na serikali yake.

Ni machafuko makubwa zaidi katika taifa hilo la visiwa lenye watu milioni 31 katika pwani ya mashariki mwa Afrika tangu Rajoelina mwenyewe aingie madarakani kwa mara ya kwanza kama kiongozi wa serikali ya mpito kufuatia mapinduzi yaliyoungwa mkono na jeshi mwaka 2009.