Jumamosi , 14th Sep , 2019

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, amewaomba waafrika msamaha pamoja na kuonesha kujuta kwake, kufuatia mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni yaliyotokea siku za hivi karibuni nchini humo na amewakaribisha raia wa mataifa mengine kwenda huko akisema hali hiyo haitotokea tena.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa

Akizungumza leo Septemba 14, 2019 wakati wa Shughuli za kutoa heshima za mwisho kwa Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe yaliyofanyika katika uwanja wa Mpira wa Harare nchini humo, Rais Ramaphosa amesema kuwa kilichotokea nchini kwake ni kinyume na taratibu za makubaliano kwa viongozi wa nchi hizo.

Rais Ramaphosa alionyesha masikitiko yake baada ya wazimbabwe kuanza kupiga mayowe, punde tu alipokaribishwa kutoa hotuba yake fupi.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, akizungumza kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, amesema kuwa Tanzania inahuzunika kama ambavyo wao wanahuzunika kwa kupoteza kiongozi shujaa na mahiri.

Mwili wa Rais huyo wa zamani wa Zimbabwe, utazikwa kwenye makaburi ya mashujaa wa kitaifa mjini Harare.