Jumanne , 17th Aug , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa ombi kwa nchi za ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kushirikiana kwa pamoja katika kuendeleza jitihada za kuwainua na kuwawezesha wanawake kwenye nchi zao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Bingu uliopo Jijini Lilongwe nchini Malawi.

Rais Samia amesema hayo leo nchini Malawi katika Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi wa Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo mwa kusini mwa Afrika SADC na kusema kuwa akiwa kama mwanachama mpya ameahidi Tanzania kuendelea kuwa muaminifu na muadilifu wa jumuiya hiyo.

"Nataka kuwasihi kaka zangu wa ukanda huu tuendelee kushirikiana katika kuendeleza jitihada za kuwainua na kuwawezesha kiuchumi na kisiasa wanawake kwenye nchi zetu," amesema Rais Samia.

Pia RAis Samia amesema licha ya jumuiya hiyo kuwa na mafanikio makubwa hapaswi kuridhika kwa kuwa bado wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kuendelea kwa hali ya umasikini, ukosefu wa ajira.

Aidha, Rais Samia ameomba jitihada za upatikanaji wa chanjo kwa ajili ya Uviko-19 kuendelezwa kwani mahitaji ya chanjo ni makubwa.

"Mahitaji ya chanjo bado ni makubwa na hatuna budi kuendelea kuongeza jitihada za upatikanaji wa chanjo na pia kuzishawishi kampuni zinazozalisha chanjo kuridhia kutoa vibali vya teknolojia, ili kuruhusu chanjo ziweze kuzalishwa sehemu nyingine," amesema Rais Samia.
 
Leo Agosti 17, 2021 Rais Samia ameshiriki kwa mara ya kwanza kwenye mkutano huo wa SADC akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.