Ijumaa , 17th Oct , 2025

Mwili huo uliotarajiwa kusafirishwa moja kwa moja hadi katika uwanja wa Nyayo, ulipelekwa bungeni ili kuwapa fursa wabunge kuuaga kabla ya kupelekwa katika uwanja wa Nyayo.

Wakati Kamati ya Kitaifa inayoratibu mazishi ya Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga ikifanya mabadiliko kwenye ratiba ya kumuaga kiongozi huyo jana Alhamis kwa kutopeleka mwili wake katika bunge la nchi hiyo, ratiba ya mazishi ya kiongozi huyo wa zamani wa taifa hilo imebadilika kwa mara nyngine leo Ijumaa Oktoba 17 baada ya mwili wake kupelekwa hadi bunge ili kuagwa na viongozi hao.

Mwili huo uliotarajiwa kusafirishwa moja kwa moja hadi katika uwanja wa Nyayo, ulipelekwa bungeni ili kuwapa fursa wabunge kuuaga kabla ya kupelekwa katika uwanja wa Nyayo.

Hapo Jana ratiba hiyo ilibadilika kwa mara ya kwanza baada ya waombolezaji kuupokea mwili wake katika uwanja wa ndege wa JKIA na kutembea nao moja kwa moja hadi Kasarani ili kuagwa.

Hii ilikuwa kinyume na ratiba hiyo ambapo ulitarajiwa kuchukuliwa kutoka JKIA, kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee kabla ya kupelekwa bungeni ili kuagwa.

Mwili huo sasa utaagwa bungeni ambapo rais atawaongoza viongozi tofauti kuuaga mwili huo huku taarifa kutoka nchini humo zikisema wabunge waliombwa kuwa maeneo ya bunge mapema leo kwa ajili ya kumuaga kabla ya mwili huo utapelekwa katika uwanja wa Nyayo ambapo ibada ya mazishi itafanyika kuanzia saa 9 asubuhi kabla ya Wakenya kumuaga tena.