RC aliyetaka Mungu amshukuru JPM atakiwa kujutia

Jumatano , 10th Apr , 2019

Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu amekosoa kauli ya  Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri kwamba Mungu anapaswa kumshukuru Rais Magufuli na kufafanua kwamba ni vyema vinywa vilindwe ili kuepuka kukufuru kwa kulewa madaraka.

RC Mwanri

Kingu amefafanua hayo ikiwa ni baada ya kusambaa mitandaoni kwa video iliyokuwa ikimuonyesha Mwanri akisema kwamba  wao wana Tabora watamuomba Mungu amshukuru Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya.

"Yeye Mungu ndio amshukuru Rais wetu na kumwambia Rais wetu asante kwa kazi anayoifanya" Alisema Mwanri.

Akiikosoa kauli hiyo Mbunge  Kingu amesema kwamba  "Tusifike mahali kama taifa na viongozi kuanza kujiinua zaidi ya Mungu. Hii litaleta laana ambayo hakuna atakayesimama juu ya kauli zinazojiinua dhidi ya Mungu. Jehova hajaribiwi wala kudhihakiwa, Mungu tupe hekima kulinda vinywa maana vimebeba uzima na mauti".

"Yahwe mkuu sana, lazima tulinde vinywa kuepuka kukufuru kwa kulewa madaraka. Kauli kuwa Mungu ndio amshukuru Rais wetu natamka wazi haina uvuvio wa Ki Mungu bali imebeba emotions za kidunia na kukosa unyenyekevu mbele ya mtoa uzima ambaye ni Yahwe na Jehoval Elishadai" amesema.

Ameongeza kwamba "yule aliyeitoa ajutie na kumwomba Mungu wa rehema kuwa aliingiliwa na mwovu katika kinywa.Mimi ni dhaifu na mwenye dhambi lakini niko chini ya Neema ya Mungu najua madhara kwa nchi kwa kauli kama hii".