Jumanne , 20th Sep , 2022

Viongozi na watendaji wa serikali katika ngazi mbalimbali mkoani Kagera, wametakiwa kuepuka kuzua mivutano pindi wanapojitokeza wawekezaji na wadau wa maendeleo kufanya uwekezaji katika maeneo ya mkoa huo 

Inaelezwa hali hiyo husababisha wahusika kuondoka na kwenda kuwekeza katika maeneo mengine yasiyo na mivutano, na kusababisha mkoa kushindwa kupiga hatua haraka za kimaendeleo.

Akizungumza katika kikao na viongozi wa jamii kuhusu chanjo ya Uviko 19 kilichokwenda sambamba na ugawaji wa pikipiki 76 kwa watumishi wa afya, zilizotolewa na mashirika ya MDH na BUDES kwa ajili ya kwenda kuhamasisha chanjo hiyo kwa jamii, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila amesema kuwa serikali haiwezi kuruhusu pesa ya maendeleo irudi kwa sababu ya mivutano.

"Tunapozungumzia mkoa uende mbele kimaendeleo ni pamoja na kuwapa moyo wadau wa maendeleo mfano hawa wa MDH na wengine ili kuyasukuma maendeleo yetu katika nyanja ya afya, ya elimu na nyinginezo, kwa sababu peke yetu hatuwezi" amesema Chalamila. 

Akizungumza katika kikao hicho kaimu mkurugenzi wa shirika la MDH Dk. Nzovu Ulega amesema kuwa kwa kushirikiana na halmashauri wamejenga vituo vya afya 50 katika mkoa wa Kagera, na kushiriki mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko 19 kwa kuhakikisha watu wote wenye sifa za kupatiwa chanjo, wanachanjwa.

"MDH inafurahi sana kuona tumefikia hatua ambayo tunaweza kuonyesha takwimu ambazo mkoa umefikia kwenye kutoa chanjo, lakini bado kuna kazi kubwa iliyo mbele yetu, na katika kikao hiki nina imani tutaondoka na mbinu mbalimbali za kujikinga na Uviko 19 na kuendelea kuhamasisha wenzetu kukijinga" amesema Dk. Ulega
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa, Kagera sasa umefikia asilimia 63 ya utoaji wa chanjo ya Uviko 19.