Jumatano , 27th Apr , 2022

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla amemtaka Mkandarasi kutoka Kampuni ya CHICO anaetekeleza Mradi wa Ujenzi wa Mto Ng'ombe wenye urefu wa Km 8.5 kurudi eneo la kazi na kukamilisha kazi iliyobaki ili lengo la Serikali kumaliza Kero ya mafuriko kwa Wananchi ikamilike.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla

RC Makalla ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya kukagua Miradi huo na kukuta Mkandarasi hayuko eneo la kazi licha ya kulipwa zaidi ya Asilimia 60 ya Fedha huku  akimuelekeza Mkandarasi kuongeza Nguvu kazi ili kazi iweze kukamilika na kukabidhiwa kabla ya November mwaka huu.

Aidha RC Makalla amebainisha kuwa Wananchi waliolipwa fidia ya zaidi ya  Shilingi Bilioni 6 na bado hawajaondoka,  RC Makalla ameelekeza wote waliolipwa kupisha Mkandarasi akamilishe kazi ambapo amesema atapita kila wiki  kukagua maendeleo ya Ujenzi.

Mkuu wa Mkoa Dar pia amewataka TARURA kumsimamia Mkandarasi huyo aanze Ujenzi wa Barabara ya mtaa huo ikiwa ni Baada ya kupokea malalamiko ya Wananchi kuhusu ubovu wa Miundombinu ya Barabara hiyo.