Jumanne , 25th Nov , 2025

RC Makame ametoa onyo kwa wafanyabiashara wote wa Mbolea Mkoa wa Songwe kutojihusisha na kuuza Mbolea ya Ruzuku nje ya mfumo

Mkuu wa Mkoa wa Songwe ndugu Jabiri Makame amefanya oparesheni ya kushtukiza na kuwakamata wafanyabiashara wa Mbolea Wilaya ya Mbozi ambao wamekuwa wakiuza Mbolea ya Ruzuku kinyume na bei elekezi ya Serikali.

Oparesheni hiyo imefanyika kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa kwake na wakulima katika Jukwaa la Wadau wa Kilimo Mkoa wa Songwe kujadili mikakati ya kuendeleza Sekta ya Kilimo Mkoani humo.

Akizungumza katika Oparesheni hiyo, RC Makame ametoa onyo kwa wafanyabiashara wote wa Mbolea Mkoa wa Songwe kutojihusisha na kuuza Mbolea ya Ruzuku nje ya mfumo, kuuza zaidi ya bei elekezi na kutothubutu kutorosha Mbolea kwenda nje ya nchi kwani Kufanya hivyo ni kudidimiza jitihada za Rais wetu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuwakomboa wakulima katika Mkoa wa Songwe.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Mbolea Kanda ya Mbeya ndugu Joshua Ng'ondya ameeleza kuwa Mkoa wa Songwe una tani 9825 za aina mbalimbali za Mbolea, Serikali imefanya jitihada na kuingiza tani 22,000 za Mbolea ya kupandia ambazo zinaendelea kusambazwa, na kwamba Serikali inahakikisha kwamba Mbolea inaendelea kupatikana katika Msimu huu wa Kilimo.