Ijumaa , 27th Jan , 2023

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima amepokea ripoti ya uchunguzi kuhusu tuhuma za kuuza viwanja vya serikali kinyume na utaratibu katika Halmashauri ya wilaya ya Nyamagana Mkoani humo

Ripoti hiyo imeandaliwa na kamati iliyoundwa ili kuchunguza tuhuma hizo zilizotolewa na wadau
Akipokea ripoti hiyo, RC Malima amesema kamati hiyo ya maadili imefanya kazi kubwa katika kufuatilia suala hilo na kuahidi kufanyia kazi yote yaliyoelezwa na kamati hiyo

"Kamati hii imekuja na ripoti hii ambayo mimi nimepatiwa kwa muhtasari kwa sababu mimi ndiyo nilielekeza kamati ifanye kazi nashukuru kamati hii wakati tunaielekeza tulikuwa kwenye mfumo wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Mwanza na haswa hoja yenyewe sababu iliibuka kwenye kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Nyamagana kwahiyo tumepata hii taarifa wamejifungia siku nane ndiyo wamekuja na ripoti yao mimi nimepata muhtasari wa taarifa hiyo"

Aidha RC malima ameagiza kufatilia migogoro yote ya ardhi katika mkoa huo kwani imekuwa tatizo linalojirudia kila mara kutokana na malalamiko ya wananchi anayopokea.

‘Inaonekana kumekuwa na taratibu za unyang’anyi wa viwanja ndani ya Mwanza unyang’anyi kabisa tunauita hivyo kwamba mtu una kiwanja chako anakuja mtu mjanja kupitia idara ya ardhi na watendaji wake unanyanganywa kiwanja chako its not fair na mara nyingi watu wanofanyiwa hivi ni watanzania wa hali ya chini na huenda ardhi ile ingekuwa ni jambo la manufaa kwake labda angeweza kuitafsiri kiuchumi kwa maana ya kuiuza kwa taratibu anazotaka yeye lakini najua kuna malalamiko ya watu wengi wanasema kuna mamlaka zinaenda kwao na kusema ardhi hii inahitajika na serikali kwahiyo wanaichukua na kuinyang’anya’

Awali akikabidhi ripoti hiyo mkurugenzi wa tume ya maadili ya viongozi kanda ya ziwa Godson Kweka, amesema wakati wakikamilisha uchunguzi huo walibaini matatizo mengine ya ardhi na hivyo kuomba kuongezewa muda wa kufanya uchunguzi zaidi.

"Katika kufanya kazi hiyo tumegundua pia kuna mambo mengine ambayo yana muelekeo wa ukiukwaji wa maadili kama ilivyo katika viwanja namba 194 na 195 kwahiyo ushuri wa kamati ni kwamba tupewe muda ili iendelee kufanyia kazi hilo"

Kamati hiyo imetumia siku nane kuchunguza kuhusu uuzwaji wa viwanja viwili vya serikali namba 194 na 195 vinavyodaiwa kuuzwa kwa shilingi bilioni 1 na kupelekea hivi karibuni mkuu wa mkoa huo wa Mwanza Adam Malima kumshtaki kwa wizara ya tamisemi mkurugenzi wa halmashauri ya jiji hilo Selemani Sekiete kwa kuuza viwanja hivyo huku watumishi wengine wanne wakisimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa uuzwaji wa viwanja hivyo.