Ijumaa , 28th Oct , 2022

Miili ya Askari wawili wa Uhamiaji waliouwawa wakati wanatekeleza majukumu yao mkoani Geita imeagwa leo mkoani humo huku Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigella akiviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya msako ili kila aliehusika na tukio hilo aweze kuwajibika.

"Awe ni kiongozi, awe mwananchi wa kawaida wote tunawakamata tunawafikisha kwenye vyombo vya sheria lakini la pili vita ya mapambano dhidi ya uhalifu katika mkoa wa Geita  haiwezi kurudi nyuma, wale wote waliohusika kuhifadhi wahamiaji wale wote wanaojihusisha na uhalifu wa aina yeyote  katika mkoa wa Geita  mapambano na ufuatiliaji wa operation mbalimbali zitaendelea kwa kasi kubwa", amesema Shigela. 

Askari hao waliuawa wakati wakiwakamata raia wa kigeni waliokuwa wamehifadhiwa kwenye nyumba ya mwananchi mmoja wa kata ya Mtakuja wikayani Mbogwe 

Wananchi waliozungumza na EATV wameomba serikali kufanya msako ili kila aliyehusika aweze kuwajibishwa
"Kwakweli tunaomba serikali ifanye kazi, huu ugaidi usijirudie tena kwa sababu kwanini wao wakienda kukamata watu hawawaui, alafu wao wanajichujulia madaraka wanawauwa ambao wakikuwa wanawakinda, kwakweli tunaomba serikali ifanye kazi" amesema Editha Kazigo mwananchi ambaye ni Jirani wa moja kati ya waliouawa

Mwakilishi wa kamishna Jenerali wa Uhamiaji Samwel Mahirani anasema hakuna mtu mwenye haki ya kumuondolea mwenzie uhai hivyo ameomba wananchi kutoa ushirikiano kwa serikali ili waliohusika waweze kukamatwa.