Jumapili , 17th Aug , 2025

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ametoa wito kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kufikisha huduma ya majisafi ya bomba katika vijiji takribani 1,500 vilivyobaki ifikapo mwaka 2030 ili huduma hiyo ipatikane katika vijiji vyote 11,353 vilivyo chini ya wakala huo

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ametoa wito kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kufikisha huduma ya majisafi ya bomba katika vijiji takribani 1,500 vilivyobaki ifikapo mwaka 2030 ili huduma hiyo ipatikane katika vijiji vyote 11,353 vinavyopaswa kuhudumiwa na Wakala huyo hapa nchini, ambapo hadi sasa jumla ya vijijini 9,894 zimefikiwa na huduma hiyo.

Ametoa wito huo Agosti 15, 2025 Mbweni Mkoani Dar es Salaam wakati akifunga kongamano la siku tano la tathimini ya RUWASA iliyofanywa na Menejimenti ya Wakala huyo ikijumuisha Mameneja wa Mikoa na kuhudhuriwa na baadhi ya wadau wake.

Waziri Aweso pia alipongeza eneo la Utoaji huduma ya Maji Vijijini linalosimamiwa na RUWASA kupitia Vyombo vya Utoaji Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) kuwa linafanya vizuri huku ukitaka nguvu zaidi ili huduma iwe endelevu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya RUWASA Mha. Ruth Koya aliishukuru Wizara ya Maji kwa kuiwekea taasisi hiyo mazingira rafiki ya kufanyia kazi hali inayosaidia utendaji wake kuwa rahisi na kupata matokeo ya haraka katika kuwahudumia wakazi wa vijijini huduma muhimu ya majisafi na salama.

Awali, akitoa maelezo kwa mgeni rasmi kuhusu kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhe. Wolta Kirita alisema katika siku tano za kongamano hilo la kujitathimini kumekuwa na mijadala ya kina kuhusu utendaji kazi wa miaka sita tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo Julai 1, 2025 na kwamba mwelekeo wa sasa ni kuimarisha zaidi eneo la usambazaji maji kwani lengo la kuanzishwa kwake ni kutoa huduma ya majisafi kwa wakazi wa maeneo ya vijijini Tanzania Bara.

Katika hatua nyingine, RUWASA imempatia zawadi ya tuzo maalum Waziri Aweso kama shukrani na kumbukumbu kwa huduma yake bora kwa taasisi hiyo na sekta ya maji kwa ujumla.