Jumanne , 19th Jul , 2016

Maandalizi ya mkutano mkuu maalum wa kumchagua mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi yamekamilika ambapo wajumbe wa Mkutano mkuu huo wamehakikishiwa usalama wa kutosha katika kipindi chote cha mkutano huo.

Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka.

Hayo yameelezwa na Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa makao makuu ya CCM mjini Dodoma na kusema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha usalama kwa wajumbe wote wa mkutano huo.

Amesema mkutano huo utatanguliwa na kikao cha sekretarieti ya Halmashauri kuu ya taifa ambacho kitakutana leo na kufuatiwa na kikao cha kamati kuu ya Halmashauri kuu ya Taifa ambayo itakutana Julai 21 ambapo kikao cha Halmashauri kuu ya Taifa kitakutana Julai 22 na kupendekeza jina la mgombea uenyekiti wa chama hicho na kulipeleka kwenye mkutano mkuu.

Amesema Mkutano mkuu maalum wa kumchagua mwenyekiti mpya wa chama cha Mapinduzi utafanyika Julai 23 mwaka huu ambapo jina la Rais Dk John Pombe Magufuli limependekezwa kugombea nafasi hiyo ambapo atapigiwa kura ya ndiyo na hapana.

Jumla ya hotel 306 na vyumba 3,331 mjini Dodoma vimeshachukuliwa kwa ajili ya wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa kumchagua mwenyekiti wa chama hicho huku ikitegemewa zaidi ya wajumbe 2,000 kuhudhuria katika mkutano huo pamoja na wageni waalikwa.

Sauti ya Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka.