
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala na Tamisemi Dk.Prudenciana Kikwembe
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki amesema serikali imeanza kufanyia kazi marekebisho ya utaratibu wa utoaji hati za kimila ambazo zimeonekana bado ni changamoto na ndio chanzo cha migogoro mingi ya ardhi nchini.
Mhe. Kairuki ameyasema jana Jijini Dar es Salaam alipokutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala na Tamisemi pamoja na uongozi wa Mpango wa Kurasimisha Biashara za Wanyonge (MKURABITA) na kuongeza ofisi yake itahakikisha mpango huo unainua vipato na kuwainua wanyonge sambamba na kuwanufaisha watanzania wote bila ubaguzi.
Mhe. Kairuki amesema ofisi yake inashirikiana na taasisi zingine zinazohusika na vibali mbalimbali kutambua uhalali kwa baadhi ya watu ambao wamekua wakijitokeza kwa madai mbalimbali hasa yale madai ya ardhi ambayo yanahusisha masuala ya uzalishaji mali kama ya Kilimo na kupunguza hali ya migogoro isiendelee kutokea.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala na Tamisemi Dk. Prudenciana Kikwembe amesema mpango wa Mkurabita unapaswa kushirikisha makundi maalum ya kinamama, wazee, watoto na walemavu nchini ili kuhakikisha wanapunguza umaskini nchini hasa maeneo yaliyosahaulika ya vijijini kwani mfuko huo umeundwa kwa ajili ya watanzania wenye hali duni kwa maeneo ya vijijini.
