Alhamisi , 29th Apr , 2021

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Amani Chande amesema utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Mto Msimbazi utaanza mara baada ya serikali kuidhinisha kuhusu matumizi ya fedha za mkopo kupitia Wizara ya Fedha na Mipango.

Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Abbas Tarimba, Kulia Sehemu ya bonde la mto Msimbazi (Picha kutoka mtandaoni)

Mhe. Chande amesema hayo leo bungeni, akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Abbas Tarimba juu ya lini serikali itaanza ujenzi wa Mto Msimbazi ambao umeainishwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025.

Amesema Serikali ina mpango wa kulibadili eneo la bonde la mto Msimbazi kuwa eneo la uwekezaji na fursa mbalimbali, na mpaka sasa usanifu wa mradi huo umekamilika.

Pia Mhe. Chande amesema kuwa ilikuhakikisha athari zinazojitokeza wakati wa mafuriko zinapungua wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wanakifanyia usafi wa mara kwa mara kipande cha Mto Msimbazi cha daraja la Jangwani.