Alhamisi , 19th Apr , 2018

Serikali ya Tanzania kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kamati za maafa zilizopo katika mkoa zitafanya tathmini ili kujua miundombinu iliyoharibika ikiwemo barabara, madaraja na miradi mbalimbali hata ile ya watu binafsi ili taratibu za matengenezo zipate kufanyiwa kazi.

Waziri Mkuu Majaliwa amebainisha hayo leo Aprili 19, 2018 Bungeni jijini Dodoma kwenye kikao cha 13 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa Wabunge mbalimbali ambayo yalikuwa yanaelekezwa kwa kwake ili yapatiwe majawabu.

"Mvua bado zinaendelea kunyesha nchini, kamati za maafa katika kila mkoa zitafanya tathimini ya kujua ni miundombinu ipi imeharibika na kwa kiasi gani pamoja na ile ya watu binafsi ili taratibu za kawaida za matengenezo zifanyike hususani na TANROAD na TARURA", amesema Majaliwa.

Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu amesema kwa sasa kumekuwepo na neema ya mvua ambayo ina nyesha maeneo mbalimbali nchini huku serikali ikiwa imeweka mikakati ya miundombinu ya kutosha katika jiji la Dar es Salaam ili kuwezesha kuimarisha njia za kupita maji na kuwataka wananchi wanaishi mabondeni kuhama ili kujiepushia kupata madhara zaidi.