Ijumaa , 19th Dec , 2025

Kwa upande wa sekta ya elimu, Dkt. Mwigulu amesema serikali imefanikisha ujenzi wa madarasa 79,000, shule mpya za sekondari zaidi ya 1,300 na shule mpya za msingi zaidi ya 2,700.

 Serikali ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya uzinduzi wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ikilenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya kwa uhakika bila vikwazo vya kifedha.

Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uyole, mkoani Mbeya ambapo amebainisha kuwa utekelezaji wa awali wa mpango huo utaanza kwa makundi ya watoto, akina mama wajawazito, na wazee. Uzinduzi rasmi unatarajiwa kufanyika Januari 2026.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Dkt. Mwigulu amesema serikali imefanikisha ujenzi wa madarasa 79,000, shule mpya za sekondari zaidi ya 1,300 na shule mpya za msingi zaidi ya 2,700. Aidha, mchakato wa ajira za walimu 7,000, wakiwemo walimu wa sayansi na hesabu, unaendelea na walitarajiwa kuanza kazi Januari 2026.

Wakati huohuo, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeelekezwa kufanya tathmini ya miradi yote iliyolipwa fedha ili kuhakikisha thamani ya fedha inalingana na kazi iliyotekelezwa. Amesisitiza kuwa wakandarasi wa miradi ya Serikali hawaruhusiwi kupeleka malipo katika akaunti za nje ya nchi, bali wanapaswa kutumia akaunti za ndani.

Pia, amewataka viongozi wa Serikali katika ngazi zote kutatua kero za wananchi kwa uwajibikaji na kwa wakati, bila urasimu usio wa lazima.

Dkt. Mwigulu amewahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Viongozi wa Serikali wametakiwa kusimamia miradi kwa uwazi, uwajibikaji na kuhakikisha thamani ya fedha inaleta manufaa kwa wananchi.