Ijumaa , 31st Mei , 2019

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Elneza Ayo, amewataka wananchi kuchemsha maji wanayotumia ikiwemo ya kupigia mswaki, ili kuhakikisha wanajitenga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.

Hayo ameyasema leo Mei 31, 2019 kwenye kipindi cha East Africa Breakfast cha East Africa Radio, wakati akizungumzia uwepo wa magonjwa ya mlipuko ikiwemo Dengue na Kipindupindu ambapo amesema serikali ya mkoa ina mpango wa kuondoa ugonjwa huo.

"Nawaomba wananchi kila maji wanayotumia wachemshe kwa sababu hatujui maji yanakopita kuna mazingira gani, nashauri mwananchi maji ya kunywa achemshe, maji ya kupikia achemshe na hata maji ya kupigia mswaki achemshe" amesema Ayo

Kuhusiana na ugonjwa wa Dengue Ayo amesema, "tuna mpango wa kupulizia dawa za ugonjwa huo kwa njia ya Helikopta ila tulisitisha mara moja kwa sababu ya mvua zinazoendelea lakini mvua zimeelekea mwishoni hivyo tutapulizia muda si mrefu ili kupunguza Dengue."

''Ni kweli gharama ni kubwa sana kutibu Dengue lakini Hospitali za Mkoa wa  Dar es salaam, matibabu yake itakuwa ni bure, lakini kwa Hospitali binafsi wenyewe watakuwa na gharama" ameongeza Ayo.

Mpaka sasa jijini Dar es salaam takribani watu wawili wameripotiwa kufa kwa ugonjwa wa Dengue, wakati ugonjwa wa Kipindupindu mtu mmoja ameripotiwa kufariki dunia.