Jumanne , 26th Jul , 2022

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, itahakikisha inaendelea kusimamia madai ya madereva pamoja na haki za waajiri katika kutekeleza madai ya madereva wa malori.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Julai 26, 2022, wakati akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Innocent Bashungwa, Waziri wa Mambo ya Ndani pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara hizo na Kamishna Jenerali ya Polisi, Camilius Wambura, kwenye jijini Dodoma.

 "Lengo ni kuhakikisha madereva wanaendelea na ajira zao na wanapata maslahi yao kwa mujibu wa sheria ili waweze kuendesha shughuli zao na familia zao na serikali itasimamia madai yao na haki za waajiri katika kutekeleza madai ya madereva wasije wakawajibika na vitu ambavyo haviko kwenye sheria zetu za nchi," amesema Waziri Mkuu
  
Katika kikao hicho ambacho pamoja na mambo mengine kililenga kujadili suala la mgomo wa madereva wa malori, Waziri Mkuu amesema awali kulikuwa na malalamiko ya madereva ambapo Serikali ilikutana na wadau wakiwemo waajiri na wamiliki wa maroli na kukubaliana masuala mbalimbali ya kutekeleza.

Amesema malalamiko ya madereva hao ni kutopewa mikataba ya kazi, kutokuwa na uhakika wa matibabu yao na familia zao (bima ya afya) na kutounganishwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili wawe na uhakika wa kupata mafao baada ya kustaafu na madai ya kutopatiwa posho mbalimbali.