Serikali yatoa tamko wanaoishi karibu na Jeshi

Jumatano , 15th Mei , 2019

Serikali imeliambia bunge kuwa wanaendelea kuwalipa fidia stahiki wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa na jeshi kwa ajili ya utekelezaji wa jukumu la ulinzi wa nchi.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi akijibu bungeni leo amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2018/19, Wizara ilitenga shilingi bilioni 20.9 kwa ajili ya  kulipa fidia maeneo yaliyotwaliwa na jeshi ambapo baada ya uhakiki tayari kiasi cha shilingi bilioni 3 kimelipwa.

Swali hilo liliulizwa na Mbunge wa Mtambile ambaye alihoji, "Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia kwa wananchi ambao maeneo yamechukuliwa na Jeshi"?.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Ulinzi, Husein Mwinyi amesema kuwa, "baadhi ya maeneo yameshalipwa na mengine mchakato unaendelea, nia ya Serikali ni kulipa fidia kadri hali ya fedha itakavyoruhusu, 2018/2019 tulitenga Bil 20.9 za kulipa fidia, baada ya uhakiki Bil 3 zimelipwa na uhakiki maeneo mengine yanaendelea".