Jumanne , 22nd Jun , 2021

Wizara ya Fedha na Mipango, imependekeza kuongeza kiasi cha shilingi bilioni 70 kitakachowawezesha takribani wanafunzi 21,000 wa elimu ya juu walioshindwa kuendelea na masomo baada ya kukosa mkopo licha ya kwamba walikuwa na sifa za kundelea na masomo hayo.

Bodi ya Mikopo

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 22, 2021, Bungeni Dodoma na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, na kuongeza kuwa kiwango hicho cha pesa kitawanufaisha wale wanafunzi 11,000 walioshindwa kuendelea na masomo kwa mwaka jana na wale wa mwaka huu wanaokadiriwa kuwa 10,000 kutokana na kukosa mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini (HESLB).

"Mwaka jana takribani wanafunzi 11,000 wale wenye sifa waliokosa masomo kwa sababu ya mkopo na wazazi wao hawana uwezo na wakabaki majumbani na mwaka huu 10,000, wanakadiriwa wangekosa mkopo, tunapendekeza kuongeza shilingi bilioni 70 kwenye zile bilioni 300 ambazo zitawapeleka wote," amesema Dkt. Waziri Nchemba.