Jumatatu , 31st Oct , 2022

Kesi namba 10 inyomkabili Diana Bundala Maarufu kama mfalme Zumaridi na wafuasi wake 8 imeshindwa kuendelea leo katika Mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Mwanza kutokana na Shahidi namba sita ambae pia ni mshtakiwa katika kesi hiyo Suzana Simon  kutoletwa Mahakamani hapo

Imeelezwa kuwa  mshtakiwa huyo amesahaulika gerezani 

Zumaridi na wafuasi wake wanakabiliwa na kesi ya kuwazuia maafisa wa serikali kutekeleza majukumu yao na kuwajeruhi Askari Polisi 

Wakili wa utetezi Linus Amri ameiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kusikiliza shauri hilo kwani wasingeweza kujitetea bila idadi ya washtakiwa kutimia 

Aidha katika shauri namba 11 linalomkabili Zumaridi dhidi ya Jamhuri, wakili wa upande wa Jamhuri Martha Mwadenya ameomba kupangwa tarehe nyingine kwani upelelezi bado haujakamilika katika shauri hilo.

Baada ya wakili huyo kudai upelelezi bado haujakamilia Hakimu mkazi mwandamizi Boniventure Lema ameiahirisha kesi hiyo hadi tarehe 14 Novemba mwaka huu itakapotajwa tena