Jumatano , 10th Dec , 2014

Mkoa wa Shinyanga umeendelea kutajwa kuwa ni moja ya mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni, vitendo vya ukatili wa kijinsia na mauaji kwa imani za kishirikina nchini.

Mkoa wa Shinyanga umeendelea kutajwa kuwa ni moja ya mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni, vitendo vya ukatili wa kijinsia na mauaji kwa imani za kishirikina nchini hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kasi ya maendeleo kuwa ndogo miongoni kwa wakazi wake.

Mwenyekiti wa dawati la jinsia na watoto makao makuu ya jeshi la Polisi Naibu Kamishina Bi. Adolphina Chialo ameyabainisha hayo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia duniani kilichofanyika kimkoa mjini Shinyanga ambapo amesema baadhi ya mambo yanayotokana na ukatili wa kijinsia kuwa ni vitendo vya ubakaji, wanawake kuzuiwa kurithi mali na kuzuiwa kumiliki ardhi huku baadhi yao wakishambuliwa na kufukuzwa kwenye makazi yao baada ya kufiwa na waume zao wakituhumiwa kuhusika na vifo vyao.

Katika maadhisho hayo yaliyoandaliwa na shirika la wanawake Tanzania (HAWA) kwa ufadhili wa shirika la umoja wa mataifa la idadi ya watu (UNFPA) Bi. Chialo amewataka wakazi wa mkoa wa Shinyanga kushirikiana na jeshi la Polisi, wanaharakati, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wengine kuibua visababishi vya ukatili wa kijinsia na kupendekeza hatua za kuchukua ili kuutokomeza mkoani humo.

Awali afisa mkurugenzi wa shirika la haki za wanawake Tanzania (HAWA) Bi. Joyce Kiria amesema iwapo vitendo vya ukatili wa kijinsia havitodhibitiwa kwa kuanza na ngazi ya familia kuna hatari ya nchi kutokuwa mahala salama pa kuishi huku baadhi ya watoto wa kike waliofika kwenye maadhimisho hayo wakishuhudia vitendo vya ukatili wa kijinsia walivyowahi kufanyiwa na kulishukuru shirika lisilo la kiserikali la Agape kwa kuwapa misaada mbalimbali ikiwemo elimu.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni na mambo mengine yanayotokana na unyanyasaji wa kijinsia kwa asilimia kubwa huku ukiongozwa na mkoa wa Mara.