Shule ya Kisimiri waeleza siri ya kuongoza kitaifa

Ijumaa , 12th Jul , 2019

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kisimiri, Valentine Tarimo, iliyoshika namba moja katika matokeo ya Kidato cha sita 2019, amesema kujituma na kufanyakazi kwa ari, ikiwa ni pamoja na kuweka mipango thabiti, ndiyo chanzo kikubwa cha kuleta ufaulu huo.

Shule ya Sekondari ya Kisimiri

Ameeleza mipango iliyothabiti ambayo huwa wanajiwekea kila mwaka, imekuwa ndiyo chachu kubwa ya maendeleo yao, ambapo kwa mwaka huu wametimiza lengo kwa asilimia 99, baada ya wanafunzi takribani 58 kupata daraja la kwanza huku wanafunzi wawili pekee wakibaki na daraja la pili.

''Huwezi amini nikikuambia unaweza ukashangaa sana, Kidato cha 6 waliomaliza ambao leo tunafurahia matokeo yao, nimekula nao sikuukuu zote, hawakwenda likizo za Krismas, Mwaka Mpya na Pasaka'', ameeleza. 

Aidha mkuu huyo wa shule ameongeza, ''Matokea yake ndio haya, ukiangalia inahitaji uwajibikaji wa hali ya juu, sisi tunaamua kutoa likizo zetu, kwa ajili ya maslahi mapana ya vijana'', alisema Mwalim Tarimo.

Aidha mwalimu Tarimo ametoa rai kwa wadau wa elimu, kuiga mfano huo wa kujitoa, lakini pia kujenga ushirikiano na uhusiano mzuri na wazazi, ili waweze kutoa ridhaa ya watoto wao, wakati wa likizo kubaki shuleni.