Shule za binafsi zapigwa marufuku kupandisha Ada

Alhamisi , 10th Jan , 2019

Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mwita Waitara amepiga marufuku kupandishwa kiholela kwa ada na michango isiyo na tija kwa shule za Umma na binafsi jambo ambalo limekuwa kero siku za hivi karibuni.

Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mwita Waitara

Akiongea leo, Januari 10 jijini Dar es salaam, Waitara amesema kumekuwepo na malalamiko mengi kipindi hiki cha shule kufunguliwa kuwa shule za binafsi zimekuwa zikitoa maelekezo ya ada kupanda bila kukubaliana na wazazi.

''TAMISEMI tumeshatoa utaratibu kwa shule zote lazima kila jambo liwe shirikishi kwa wazazi, kama ni ada au mchango lazima kuwepo na majadiliano na makubaliano ya kikao bila hivyo ni kuvunja utaratibu'', amesema.

Waitara amesisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa wale wote wanaokiuka maelekezo ya serikali ikiwemo kutowahusisha wazazi katika kupandisha ada jambo ambalo linatakiwa lifanyike kabla ya shule kufungwa na sio ghafla tu wakati wa shule kufunguliwa.

Mbali na hilo Waitara ametoa siku 90 (miezi mitatu), kwa wazazi kuweza kupeleka watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule za serikali na endapo hawatafanya hivyo nafasi hizo zitabaki wazi au zitachukuliwa na wengine.